Friday, December 30, 2011

Serikali: Al-Shabaab wanashirikiana na wenyeji akina X-Paster mwenye Al Jihad Islamic

Al-Shabaab
Waziri Shamsi Nahodha
Kupitia safu hii, tumehakikisha tunawaletea siri za ndani kabisa kuhusu kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Umeshaona jinsi kundi hilo hatari Afrika Mashariki linavyofanya kazi na namna vijana wa Kitanzania wanavyojiunga nalo.
Kubaini yote hayo, uliona jinsi kijana, Aizak Ibnu, 20, alivyosimulia namna yeye na wenzake 24, walivyojiunga na Al-Shabaab lakini 23 walipoteza maisha.

Ipo hatari ya Al-Shabaab kuvamia Tanzania kama ambavyo wamefanya Kenya. Kutokana na tishio hilo, wiki iliyopita, mwandishi wa makala haya, alifanya mahojiano na viongozi wenye mamlaka ya usalama wa nchi.
Waliozungumza ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.
Wote walisema kuwa wananchi wawe makini kwa sababu Al-Shabaab hushirikiana na wenyeji kufanikisha uhalifu wao.
WAZIRI NAHODHA
Waziri Nahodha alikiri kuwa Al-Shabaab ni hatari, hivyo akawatahadharisha wananchi kuwa makini kwa sababu kundi hilo lina mtandao mpana ndani ya Afrika Mashariki.
“Wananchi wahakikishe  wanachukua tahadhari kila sehemu na kutoa taarifa katika vyombo vya dola wakimuona mtu ambaye wana wasiwasi naye.

“Ni vema kuchukua tahadhari mapema na nichukue nafasi hii kuwaomba wananchi kuwa macho kuhusu kikundi hicho. Niwahakikishie kwamba nimewaagiza askari wa idara ya uhamiaji kuhakikisha ulinzi unaimarishwa mipakani.
“Nimewaagiza pia askari polisi kwa kushirikiana na wananchi kupitia polisi jamii, kuhakikisha wanawakamata watu wa mtandao huo popote pale walipo na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Nahodha.


Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Waziri Nahodha  baada ya kupata habari ya vijana wa Kitanzania kupelekwa Somalia kujiunga na Al-Shabaab, aliliagiza jeshi lake  kufanya  mahojiano na Aizak.

Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema polisi wa kimataifa (Interpol) wanaendelea kuchunguza ili kujua jinsi vijana wa Kitanzania wanavyochukuliwa kupelekwa Somalia na wameanza kuwafuatilia wale wote wanaohusika.

DCI MANUMBA
Naye DCI Manumba ametahadharisha kuhusu kikundi hicho cha kigaidi  kwa kueleza kwamba nchi zote za Afrika zimeshaonja matukio ya uhalifu wao.

“Tunapotoa tahadhari kwa wananchi, lengo ni kuwakumbusha kuwa watu hao wapo Afrika Mashariki yote. Hivi sasa Somalia hakuna serikali imara kwa sababu yao,” alisema Manumba na kuongeza:

“Huu ni uhalifu wa kimataifa na umesambaa katika kila nchi na siyo rahisi kuwatofautisha na Al Qaeda, mara nyingi magaidi wamekuwa wakishirikiana na wenyeji wa nchi wanazoshambulia, kwa hiyo tuwe macho.”

No comments:

Post a Comment