Sunday, December 18, 2011

****HATARI**** Al Shabaab yaanza kazi ya Ugaidi



Na Mwandishi Wetu
TAIFA linapita katika kipindi kigumu, mtafaruku wa sakata la Katiba Mpya, ufisadi Wizara ya Nishati na Madini, tishio la kujichomeka nchini kundi hatari la Wasomali, Al Shabaab, migogoro ya wanafunzi, wamachinga, ardhi na mengine yote lakini yanabaki nusu shari.

Shari kamili ni ujumbe mkali kutoka kwa waasi uliotumwa kwa viongozi wa nchi, wakiwataka kuachia madaraka ndani ya siku 100, vinginevyo watawaondoa kwa nguvu.

Habari za ndani zinasema kuwa ujumbe huo hatari, umetumwa kupitia waraka pepe na SMS kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, wakimpa siku 100 awe ameachia madaraka, vinginevyo wahusika watatumia nguvu.
Ujumbe huo, umeelekezwa pia kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema kuwa serikali inafanya uchunguzi kuweza kuwabaini wahusika na kuwataka wananchi watoe ushirikiano.

Imeelezwa kuwa waraka huo umetumwa na kiongozi wa kikundi cha watu 2,858 ambacho kimejitambulisha kwamba kinatokana na muungano wa askari waajiriwa kutoka majeshi mawili nchini.

Katika madai yao ya msingi, kikundi hicho kinadai kuwa viongozi waliopo madarakani wameshindwa kazi ya kuongoza nchi, hivyo wamewapa siku 100 waondoke, vinginevyo watatumia nguvu kuwaondoa.

“Jeshi la polisi limeanza kufanya uchunguzi kubaini watu hao na wakipatikana tuanze kuwahoji ili hatua zichukuliwe,” alisema Nahodha.

Nakala ya waraka huo wa vitisho ulitumwa pia kwa Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Idara ya Usalama wa Taifa Makao Makuu, Wizara ya Mambo ya Nje, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na ubalozi wa Marekani Tanzania.

Nakala nyingine zimetumwa kwa Kamanda Mkuu wa Al Shabaab, ubalozi wa Uingereza Tanzania, Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya Tanzania pamoja na vyombo vya habari.

HOFU YATANDA
Wakati vitisho hivyo vinatokea, kikundi cha Al Shabaab kinachotikisa nchi za Somalia na Kenya, kinatajwa kuweka kambi Dar es Salaam na kuendesha mafunzo ya ugaidi ili kuandaa mapambano ya kile wanachokiita Jihad ya kuihami Dini ya Kiislam.


Tayari jeshi la polisi nchini linawashikilia watu kadhaa wanaojihusisha kwa namna mbalimbali na harakati za Al Shabaab.
Sakata la Katiba Mpya nalo ni kizungumkuti, kwani kwa sura pana, linaelekea kuipeleka nchi kwenye machafuko.

Tayari viongozi kadhaa wa serikali wameshatoa tuhuma kwamba kuna matajiri wanaomwaga fedha ili kufadhili vurugu mbalimbali zinazochagizwa na migomo, maandamano na kadhalika.

Rais Kikwete, alipohutubia taifa mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia wazee wa Dar es Salaam alisema, kuna watu hawaitakii mema nchi ndiyo maana hata dhamira njema ya kuihuisha katiba, wanaikataa na kutaka kuitisha maandamano.

“Walisema Uchaguzi Mkuu 2015 bila Katiba Mpya patakuwa hapatoshi, sasa tunataka patoshe bado matatizo, jamani uongozi ni kazi kweli,” alisema JK.

Hotuba hiyo ya JK, inafuatia kauli mbalimbali za baadhi ya viongozi wa kisiasa na wanaharakati waliotoa tamko kuwa endapo muswada wa kuundwa kamati ya kusimamia maoni ya wananchi kuhusu utunzi wa katiba, itapishwa na bunge, wataingia mtaani kudai haki kwa maandamano.

Ijumaa iliyopita, bunge lilipitisha muswada huo, hivyo kuufanya kuwa sheria.

Wakati ghasia hizo zikiendelea, serikali inapitia kipindi kigumu kutokana na kitimtimu cha Wizara ya Nishati na Madini, kilichoanzia kama skendo ya rushwa kwenye Bunge la Bajeti la mwaka 2011-2012, ikimgonga aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, David Jairo.

Kutokana na jitihada za Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh kumsafisha Jairo na skendo ya kukusanya shilingi bilioni moja ili kuwahonga wabunge waweze kupitisha bajeti ya wizara yake, Jumamosi iliyopita yaliibuka makubwa zaidi.

Kamati Teule ya Bunge, ilisoma ripoti yake na kueleza kubaini ufisadi wa fedha za serikali, hivyo kutoa mapendekezo kwamba Jairo, Luhanjo, Utouh na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wachukuliwe hatua zinazofaa.

Ilibainishwa ndani ya ripoti kuwa kuna skendo ya kughushi fedha iliyofanywa na Jairo kwa kuandika kiasi kikubwa kuliko malipo yaliyofanyika, jambo ambalo ni kosa la jinai.

Baada ya ripoti hiyo, wabunge walikuja juu kwa kutaka wahusika wafukuzwe na wafikishwe mahakamani na kubainisha kwamba uozo huo ni sehemu ya ufisadi wa mabilioni ya shilingi yanayokwapuliwa kila kukicha serikalini.

Katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, Jairo alikutwa na hatia ya kukusanya fedha kinyume cha utaratibu pamoja na udanganyifu wa malipo.

Skendo hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo aliyesoma bungeni barua ya Jairo kwenda kwa wakuu wa idara zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini, akielekeza kila moja itoe mchango wa shilingi milioni 50 ili kurahisisha kupita kwa bajeti ya wizara hiyo.

Ikaelezwa kuwa idara 20 zilichangia, hivyo kufanya zipatikane jumla ya shilingi bilioni moja ambazo inadaiwa lilikuwa ni fungu la kutoa rushwa kwa wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

KUTOKA UWAZI
Amani yetu ni tunu. Tunawataka Watanzania wote kusimama kidete katika kutetea amani ya nchi yetu. Uasi na vita siyo suluhu ya matatizo yetu. 

Tunaomba vyombo vyote vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake inavyotakiwa na kuwabaini wote wanaotaka kuhatarisha amani ya nchi yetu, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu sheria. MHARIRI.

No comments:

Post a Comment