Thursday, December 15, 2011

Mtanzania aliyejiunga na Al Shabaab afukuzwa kwao

WIKI mbili zilizopita tuliwaletea habari jinsi Watanzania  wanavyojiunga na wapiganaji wa kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab.

Ilikuwa tuendelee kuwaletea mfululizo huu lakini wiki iliyopita matatizo yaliyo nje ya uwezo wetu yalifanya tushindwe kuwaletea makala haya.

Katika toleo hili tumeamua kuwaletea mahojiano  yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kati ya mwandishi wa makala haya  na Aizak Abnu ILah (20) ambaye anaeleza sababu  zilizofanya afukuzwe nyumbani kwao na kwa sasa yuko wapi na anafanya nini.

 Kijana Ilah ni kati ya vijana 25 waliojiunga na Al Shabab ambapo 23 waliuawa na kubakia wawili, waliomua kutoroka na kurejea nchini Tanzania.

Hivi karibuni baada ya kuponea chupuchupu kuuawa katika  mapigano makali huko Somalia kati ya majeshi ya serikali  ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa (UN) dhidi ya Kundi la Al Shaabab, kijana huyo akiwa jijini Dar alianza kueleza kama ifuatavyo:

“Sikutegemea kama wazazi wangu wangenitimua nyumbani kama ilivyotokea, kitendo hicho kiliniumiza sana wakati fulani nikikumbuka machozi yananitoka, naonekana kama yatima wakati walionizaa bado wapo hai.

“Nilinusurika kuuawa nchini Somalia, niliamua kutoroka na kurejea nchini. “Nilikwenda kwa wazazi wangu, waliniuliza maswali mengi kwani siku nyingi tulikuwa hatujaonana na wala kuwasiliana. Kwa kifupi hawakujua nilipokuwa.

“Walijua nipo Pakstani naendelea na mafunzo ya kidini. Kwa kweli maneno niliyowasilimulia yaliwatoa machozi, kwa upande wangu niliwaeleza suala la kubadili dini jambo ambalo halikuwafurahisha.

“Walinikataza na  kunisihi kutofanya hivyo nikawa na madhehebu mawili  tofauti, kwa upande wangu niliona ni vigumu, nilibakia  katika msimamo wangu huo. 

“Ingawa katika dhehebu la wazazi wangu ni zuri lakini  nilichukizwa na kitendo cha kuua watoto na watu wasio na hatia huku ikidaiwa kwamba kufanya hivyo ni kwenda peponi.

“Najua dini ya baba ni nzuri ila kuna kikundi kidogo  kinachoamini hivyo na kuua watu na wapo  waumini katika dhehebu hilo ambao wanapinga mauaji hayo  pamoja na hayo nimeamua kubadili dini.

“Wazazi hawakufurahishwa na kitendo changu cha  kubadili dini waliamua kunifukuza nyumbani. Hata hivyo, sikubadili msimamo wangu nikaamua kutoweka nyumbani, kwa sasa sina makazi maalum lakini  naamini Mungu yupo atanisaidia.

“Nimeshaongea na viongozi wa juu wa dhehebu  nililohamia na mpango umeshafanywa, natarajia kwenda Nairobi, Kenya kusomea uongozi katika dhehebu   nililohamia.

“Nawashauri wazazi wawe makini na watoto wao wanaoaga kuwa wanaenda sehemu ambayo hawana uhakika nayo au watu kuwarubuni kwamba wawape watoto wao ili wakawasomeshe, pia viongozi wa dini waache kufundisha  vijana kupigana na kuua watu.”

Wiki ijayo mwandishi wa makala haya atakuletea hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Shamsi Vuai Nahodha kuhusiana na kikundi cha Al Shaabab na wale wote wanaojihusisha na utoroshaji vijana wa Kitanzania kwenda kupewa mafunzo nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment